Saturday, 24 September 2016

KANUSHO: PROFESA MUHONGO KUCHANGISHA SHILINGI 40,000 KWA AJILI YA TETEMEKO KAGERA


Gazeti la Mwananchi la tarehe 23 Septemba, 2016 katika ukurasa wake wa Tano imeandikwa habari yenye kichwa cha habari “Harambee ya Profesa Muhongo yakusanya Sh 40,000 Bukoba”.
Mwandishi wa Habari hiyo ameandika kuwa ziara aliyoifanya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo katika Kata ya Hamugembe, Bukoba wakati akikagua miundombinu ya umeme, iligeuka kuwa harambee baada ya waathirika wa tetemeko la ardhi kudai msaada wa chakula na mahema.
Tunapenda kuuarifu Umma wa Watanzania kuwa, siyo kweli kwamba Profesa Muhongo aliitisha harambee ya kuchangia maafa hayo kama ilivyoandikwa na Mwandishi ambaye kwa sababu zake binafsi aliamua kupindisha ukweli na kueleza kuwa, “ilimlazimu Profesa Muhongo kuitisha mchango wa fedha kutoka kwa maofisa aliokuwa ameambatana nao na kufanikiwa kupata shilingi 40,000 na kuwakabidhi wakazi hao”.
Ikumbukwe kuwa Waziri wa Nishati na Madini alikuwa mkoani Kagera kukagua shughuli za kiutafiti zinazofanywa na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi tarehe 10 Septemba, 2016 na kusababisha athari mbalimbali ikiwemo kwa miundombinu ya umeme.
Hivyo, taarifa kuwa Profesa Muhongo aliitisha harambee ya kuchangisha fedha za kusaidia waathirika wa maafa siyo sahihi kwani Profesa Muhongo hakuomba wala kuagiza Maofisa alioambatana nao kuchangia fedha kama ambavyo mwandishi anataka kuwaaminisha wananchi.
Akiwa katika kata ya Hamugembe mkoani humo ambapo alikwenda kukagua nyumba ambazo zimekatiwa huduma ya umeme kwa sababu ya kuathiriwa na tetemeko hilo, baadhi ya wananchi walidai kuwa shida yao ni chakula na malazi, na mmoja wa wananchi alisema kuwa Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kagera aliyeambatana na Profesa Muhongo, alishafika kata hiyo na kuwasaidia kiasi cha fedha.
Hata hivyo, Profesa Muhongo aliwaeleza wananchi hao kuwa, yeye alikwenda hapo kwa ajili ya kushughulikia masuala ya kitaalam anayoyasimamia na kwamba kilio chao kuhusu kucheleweshewa huduma atakifikisha kwenye Kamati inayoshughulikia Maafa aliyokutana nayo tarehe 22 Septemba, 2016.
Baada ya wananchi kumtaja Meneja wa TANESCO wa Mkoa Kagera aliyewahi kuwasaidia wananchi hao fedha kutokana na tetemeko hilo, Meneja huyo aliamua kuongeza kiasi cha Fedha na kumpa mmoja wa wananchi hao, tofauti na ilivyoandikwa kwenye gazeti kuwa Waziri wa Nishati na Madini ndiye aliyekabidhi pesa kwa wananchi.
Tunawaasa waandishi wa habari kuzingatia ukweli na usahihi katika uandishi wa habari ili kupeleka habari sahihi kwa wananchi.
Imetolewa na;
WIZARA YA NISHATI NA MADINI

No comments:

Post a Comment