Thursday, 3 March 2016

WANANCHI WA NJOMBE WAASWA KUCHANGAMKIA FURSA ZILIZOPO LINGANGA NA MCHUCHUMA

 Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu,  Jenista Mhagama akizungumza na makundi mbalimbali mara baada ya waziri huyo kufanya ziara  mkoani njombe katika eneo la mchuchuma na linganga katika wilaya ya Ludewa.
Baadhi ya wananchi na viongozi mbalimbali waliofika wilayani Ludewa kumsikiliza Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu,  Jenista Mhagama.


Njombe Mmejiandaaje fursa zilizopo kwenye Migodi ya Liganga na Mchuchuma?, swali hilo limehojiwa na Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu,  Jenista Mhagama alipofanya  ziara Mkoani Njombe lengo kuu la ziara hiyo ikiwa ni kuhabarisha kuhusu  fursa za kujiajiri zilizopo kwenye Mkoa huo. Waziri huyo amesema kuwa Mkoa wa Njombe ni moja kati ya Mikoa yenye fursa kubwa ya uwekezaji ambayo fursa hiyo ni migodi ya Makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma  iliyopo katika Wilaya ya Ludewa ambayo inatarajia kutoa ajira rasmi  zaidi ya Elfu Thelathini.

akizungumza  na baadhi ya makundi ya Vijana wa Bodaboda, Kundi la Vijana Wafyatua tofali, Walemavu wasiosikia (Viziwi), na Vikundi vya ujasiriamali kwa kina mama (VICOBA) Waziri Mhagama amesema kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu imepewa dhamana ya kushughulikia nguzo tisa za kuwawezesha Wananchi Kiuchumi uliozinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu lengo kubwa ikiwa ni ifikapo 2020- 2025 Wananchi wawe wamefika kumiliki uchumi wao  wenyewe.

“Kutakuwa na mahitaji mengi sana katika Migodi hiyo ya Liganga na Mchuchuma. Tutahitaji mashine kwa ajili ya kusaga nafaka, tutaitaji vyakula vya aina mbalimbali, tutaitaji kina mama lishe na biashara nyingine ndogo ndogo za kila aina hizo zote ni fursa za kutuwezesha sisi kujiajiri na kukuza kipato chetu.Hivyo ni vizuri kila mtu aweze kuona ni kwa namna gani anaweza kunufaika na fursa hizo zilizopo mbele yake” Alisema waziri huyo.

Vilevile amesema kuwa ili kuwezesha Wananchi Kiuchumi ipo fursa za kila Halmashauri kutengeneza Madawati ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambapo wateuliwa watapewa mafunzo ambayo yatawasaidia kuwaelimisha na kuwasimamia wananchi ili wananchi waweze kushika uchumi wao wenyewe.

Aidha amesema kuwa kundi la Madereva bodaboda ni miongoni mwa makundi muhimu yatakayonufaika na dawati hilo.
Tunatambua kuwa Madereva  bodaboda  wengi wanaondesha pikipiki si wamiliki halali wa pikipiki hizo wengi wao wanafanya kama vibarua na wengi wameshindwa kumiliki bodaboda zao wenyewe kutokana  na kuwepo kwa  masharti magumu ya uchukuaji mikopo jambo ambalo limekuwa ni kikwazo kikubwa kwao.

Hivyo program hii inalenga kuwafanya Vijana wamiliki Bodaboda zao wenyewe sharti kubwa ya program ikiwa ni Vijana kujiunga na Saccos za Vijana ili waweze kupata Mkopo wenye riba nafuu ikiwa riba  ni asilimia tisa (9%) hadi asilimia kumi(10%) mkopo ukiwa  wa mwaka mzima na baada ya hapo kijana atamiliki bodaboda yake mwenyewe.

Lakini pia program hii itawanufaisha madereva kwani wataweza kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii na kufanya utaratibu wa kupata matibabu pindi watakapopata ajali wawapo kazini.

Akiongelea swala la VICOBA kwa kina mama amesema kuwa Serikali imeingia Mkataba na Benki ya Posta ambapo kina mama watapata mikopo kwa riba nafuu ambayo itasaidida wanawake wengi kujiajiri.

Akitoa Maagizo kwenye ziara hiyo waziri huyo ameziagiza Halmashauri zote mkoani  Njombe kuhakikisha kuwa swala la ajira kwa vijana linakuwa moja kati ya agenda za kudumu kwenye Halmashauri zao, na kila Halmashauri ihakikishe inatenga maeneo kwa shughuli mbalimbali za Vijana. Hii itasaidia azma ya serikali ya kuwafanya vijana kujiajiri iweze kutekelezeka lengo kuu ikiwa ni kutokomeza tatizo la ajira kwa vijana ambalo limekuwa tatizo kwa nchi na duniani kwa ujumla.

Pia ameziagiza Halmashauri Mkoani Njombe kuhakikisha kuwa zinafungua SACCOS za vijana ambazo zitasaidia upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu na Maafisa Ushirika wakague kama SACCOS hizo zipo hai na zinafanya kazi kwa faida ya Mkoa na Vijana kwa ujumla.

 Nae Mwakilishi wa kikundi cha viziwi kutoka Njombe  alitoa kilio chake kwa  waziri kuwa Halmashauri iteue mwakilishi atakayeshughulikia maswala ya walemavu ili nao waweze kushiriki kikamilifu katika fursa hizi za kuwawezesha vijana kujiajiri  na endapo jambo hili litashindikana itakuwa ni sawa sawa na bure kwani nao wanahitaji kufaidika na fursa zilizopo.

Waziri huyo pia ameahidi kuhakikisha kuwa atajitahidi kuwasiliana na wahusika ili kuona ni namna gani wataweza kutatua kero mbalimbali wanazokumbana nazo vijana wanaojiajiri katika shughuli mbalimbali likiwemo swala la kuhakikisha kuwa  katika ngazi ya Mikoa taasisi nyingi za maendeleo ziweze kuwa na matawi ili kurahisisha utendaji kazi na kupunguza gharama za watu kufuata hudumu maeneo ya mbali pia Ameahidi huzichukua na kuzifanyia kazi baadhi ya changamoto zilizowasilishwa na makundi mbalimbali katika ziara hiyo.
IMETOLEWA NA;
AFISA HABARI HALMASHAURI YA MJI NJOMBE

No comments:

Post a Comment