Thursday, 3 March 2016

DK. KAMANI AKUBALI UTENDAJI KAZI WA MBUNGE WA BUSEGA DK. CHEGENI, AKIRI WANANCHI HAWAKUKOSEA KUMCHAGUA


Mbunge wa Busega Dkt Raphael Chegeni (kushoto) na Mbunge wa zamni wa jimbo hilo, Dkt Titus Kamani ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Simiyu walipotaza rasmi kuzika tofauti zao na kushirikiana kuleta maendeleo kwenye jimbo hilo. Pichani viongozi hao walipowadhihirishia wananchi kuwa hawana chuki wala ugomvi tena na kuwa uchaguzi umekwisha, katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa kwenye kijiji cha Lamadi wilayni Busega Machi 2, 2016.

ALIYEKUWA Mbunge wa Jimbo la Busega,Dk Titus Kamani amekubali utendaji kazi wa Mbunge wa sasa wa Jimbo hilo,Dk Raphael Chegeni,akidai kwamba wananchi hawakukosea kumchagua.

Dk Kamani aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji mdogo wa Lamadi Wilayani Busega ambao pia Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa alikuwepo .Dk Kamani,amekiri kwamba Dk Chegeni ni mchapakazi na wananchi wa jimbo hilo hawakukosea kumchagua na kwamba anamuunga mkono katika hatua zote anazofanya za kuleta maendeleo jimboni hapo.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wananchi wangu uchaguzi ulishakwisha na sasa nimeamini mmepata mbunge makini na mchapakazi ,nimetambua sasa kuwa sikustahili kupingana naye ,nitashirikiana naye katika kazi wana busega ni wamoja na wanaCCM tunajenga nyumba moja hatuna haja ya kutokubaliana ikiwa tunaona aliyechaguliwa anafanya kazi nzuri,”alisema Dk Kamani.

Alisema wananchi wa Busega wanampenda Dk Chegeni na CCM kwa ujumla hivyo ni wajibu wa viongozi wengine kumuunga mkono ili kusaidia wananchi wa jimbo hilo na mkoa wa Simiyu kwa ujumla.“Huyu bwana kweli mchapakazi,nilikosea njia kupingana naye sasa namkubali rasmi naona muda mfupi tangu aingie madarakani Busega imeanza kubadilika na mambo yanaenda,wanabusega Chegeni ni Jembe,tufanyeni kazi hakuna uchaguzi hapa umshakwisha,”alisema Dk Kamani.

Kwa upande wake Dk Chegeni alieleza kuwa tofauti zao zilishakwisha na sasa wanafanya kazi ila amefurahi kuona kwamba Dk Kamani ametambua utendaji wake na kuahidi kuendelea kufanya kazi ya kuwatumikia wanabusega.

No comments:

Post a Comment