Wednesday, 24 February 2016

Waziri Muhongo aitaka TPDC na wabia kuongeza kasi katika uwekezaji wa Kiwanda cha Gesi Kimiminika

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam 

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo ametaka kasi iongezwe katika mradi wa ujenzi wa kiwanda cha uchakataji na usindikaji wa gesi kimiminika unaotarajiwa kuanza mkoani Lindi mara baada ya taratibu za maandalizi kukamilika.
Profesa Muhongo alisema hayo katika kikao kwa ajili ya kujadili hatua iliyofikiwa  ya maandalizi  ya ujenzi  wa kiwanda hicho kilichoshirikisha watekelezaji wa mradi huo ambao ni Shirika la Maendeleo  ya Petroli Nchini (TPDC) na makampuni yanayojishughulisha na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi  nchini.

Makampuni ya utafiti wa mafuta na gesi yanayotekeleza mradi huo ni pamoja na Shell, Statoil, Ophir Energy, Pavilion na Exxon Mobil. Pia kikao hicho kilishirikisha watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST)

Mara baada ya kupokea  taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata na kusindika  gesi kimiminika Profesa Muhongo alilitaka shirika la TPDC kushirikiana kwa karibu na makampuni ya  utafiti wa mafuta na gesi yanayotekeleza mradi huo na kwa kasi  ya haraka ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati.

Profesa Muhongo alisema  Tanzania ina utajiri mkubwa wa gesi hivyo ni vyema watekelezaji  wakachangamkia  fursa hiyo ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata na kusindika gesi kimiminika ambayo  mahitaji yake ni makubwa  duniani hususan katika  bara la Asia.

“Ifikapo mwaka 2025 inategemewa kuwa mahitaji  ya  gesi  duniani  yatakuwa ni kiasi cha tani milioni 440 kwa mwaka hususan katika nchi za Asia ambazo ni karibu na Afrika, hii ni fursa ambayo tunatakiwa kuichangamkia ili kuendana na  soko  itakapofika kipindi hicho,” alisema Profesa Muhongo.

Profesa Muhongo aliendelea kusema kuwa  gesi  ya kimiminika imekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi zinazoendelea huku akitolea mfano wa Algeria ambayo ni nchi ya kwanza duniani kwa kuwa na kiwanda cha kuchakata na kusindika  gesi  kimimika ambayo kwa  sasa imepiga hatua kubwa  kimaendeleo.

Katika maandalizi ya awali ya mradi huo, Profesa Muhongo aliagiza uundwaji wa timu kwa ajili ya maandalizi ya mradi huo  ikishirikisha wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya  Fedha, Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), taasisi mbalimbali pamoja na wawakilishi kutoka katika makampuni  yanatofanya utafiti wa gesi na mafuta nchini ambayo ni mtekelezaji wa mradi huo.

Alisisitiza kuwa ni vyema timu hiyo ikawa na wataalam wenye uzoefu mkubwa watakaofanya kazi kwa weledi na kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.

Aliagiza kuwa timu hiyo kukamilisha taratibu zote za maandalizi kabla ya mwezi Novemba, mwaka huu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji kutoka Shirika la Maendeleo  ya Petroli  Tanzania (TPDC) Dkt. James Mataragio alisema kuwa shirika  lake limekuwa likishirikiana na wabia wa ujenzi wa kiwanda hicho  katika hatua zote za maandalizi  ya awali na kuahidi kuongeza kasi  ili kazi hiyo iweze kukamilika kwa wakati.

No comments:

Post a Comment