Wednesday, 24 February 2016

PROF. MBARAWA AITAKA KADCO KUONGEZA MAPATO YA SERIKALI

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akielekea kukagua ujenzi wa njia za kuruka na kutua ndege mara baada ya kukagua hanga la uwanja huo. Katikati ni Mkurugenzi wa Via Avaiation Bi. Susan Mashibe ambaye ni Muwekezaji wa Hanga hilo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akijadiliana jambo na Mkurugenzi wa Via Avaiation Bi. Susan Mashibe ambaye ni Muwekezaji wa Hanga katika Uwanja wa Ndege wa KIA. 
Muonekano wa Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa KIA mkoani Kilimanjaro unaojengwa njia za kutua na kuruka ndege na kukarabatiwa jengo la abiria. Ujenzi huo unafanywa na kampuni ya NACO kutoka Uholanzi.
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa KIA mkoani Kilimanjaro.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Arusha, Eng. John Kalupale (wa pili kulia) akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kushoto) kuhusu ujenzi wa barabara ya Kia-Mererani yenye urefu wa Km 26 unavyoendelea.
Muonekano wa moja ya makalvati makubwa yaliyojengwa katika barabara ya Kia-Mererani yenye urefu wa Km 26. 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akifafanua jambo kwa Mhandisi Mshauri anayesimamia mradi wa ujenzi wa barabara ya Kia-Mererani Km 26.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kushoto) akikagua karakana ya Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA mkoani Manyara.

Serikali imeitaka kampuni ya KADCO inayoendesha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kuongeza mapato na kuimarisha ulinzi ili kulinda hadhi ya uwanja huo, kuchangia pato la serikali na kudhibiti hujuma dhidi ya watu wasio waaminifu. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema hayo wakati akikagua utendaji wa uwanja huo na mradi wa ujenzi wa njia za kurukia ndege na jengo la abiria unaondelea katika uwanja huo.

Prof. Mbarawa amemtaka Kaimu Mkurugenzi wa KADCO Bw. Bakari Mururusi, kuhakikisha kuwa uwanja huo kuanzia mwaka huu wa fedha unazalisha mapato yanayowiana na hadhi yake na kuchangia kikamilifu mapato ya Serikali na kuachana na utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea.

“Siridhiki na kiasi cha bilioni 18 mnazozalisha kwa mwaka, nawataka kuanzia sasa mkusanye mapato ya kutosha na kudhibiti vitendo vya hujuma ili kuupa hadhi inayostahili uwanja huu”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Amemtaka Muwekezaji wa Hanga (garage) la Uwanja huo kujiandaa kuondoka kutokana na kutowekeza kikamilifu katika kipindi cha miaka 10 alichokodishiwa na kusisitiza kuwa nia ya Serikali ni kukabidhi hanga hilo kwa Shirika la Ndege nchini (ATCL), ifikapo Julai mwaka huu ili lifanye kazi kwa faida na madhumuni yaliyokusudiwa.

“Nia ya Rais ni kufufua ATCL liwe na hadhi inayoshatahili hivyo hanga hili tutawapa ATCL na kuwasimamia ili wafanye kazi kikamilifu na kuleta mapato kwa Serikali”, amefafanua Waziri Prof. Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa amemweleza Mkurugenzi wa Kampuni ya Via Aviation inayomiliki hanga hilo kwa miaka 10 kuwa Serikali hairidhishwi na mapato yanayotokana na hanga hilo hivyo imejipanga kuitumia kuleta faida zaidi kwa Serikali katika mkakati wake wa kukuza uchumi.

Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Kia-Mererani yenye urefu wa Km 26 inayojengwa na Kampuni ya Chicco kwa gharama ya shilingi bilioni 32.2 na kumtaka mkandarasi huyo kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Manyara, Eng. Yohani Kasaini amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa licha ya barabara hiyo kupita katika ukanda wa tambarare jumla ya makalavati makubwa 6 na madogo 85 yanajengwa ili kukabiliana na changamoto ya mafuriko na hivyo kuiwezesha barabara hiyo kupitika wakati wote wa mwaka.

Barabara ya Kia-Mererani ina umuhimu wa kipekee kiuchumi kwani inapita katika ukanda wenye rasilimali zenye madini ya Tanzanite, eneo zuri la kilimo, ufugaji, utalii na misitu hivyo kukamilika kwake kutapunguza gharama za usafiri na kuvutia watalii wengi kuja nchini.

Serikali iko katika mkakati wa kuimarisha uwanja wa ndege wa KIA kwa kukarabati jengo la abiria na njia za kutulia na kurukia ndege ambapo kampuni ya NACO kutoka Uholanzi inajenga uwanja huo ili kuuwezesha kufanya kazi kisasa, kuruhusu ndege nyingi kutua na kuongeza mapato ya uwanja huo na Serikali kwa ujumla.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amewataka watendaji wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo mkoani Manyara kufanyakaz kwa umoja, uwazi, uadilifu ili kuiwezesha lengo la wizara hiyo la kujenga miundombinu itakayoliwezesha taifa kufikia uchumi wa kati 2025 kutimia kwa wakati.

No comments:

Post a Comment