Na Chalila Kibuda, Globu ya jamii
SERIKALI imetoa miezi mitatu kwa watu wanaomiliki viwanja kwa ofa ya jiji ili kuweza kupata hati baada ya kubainika kuwepo kwa matapeli wa kugushi nyaraka za serikali kwa viwanja hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesesema katika uhakiki huo wameweza kubaini Raia mwenye asili ya Asia, Hamant Patel kumiliki ardhi kwa viwanja vitano katika mikoa mitatu.
Amesema kuwa waliopewa viwanja kwa ofa ya jiji, hati hizo zitatolewa na Kamishina wa ardhi na watakaobainika kugushi nyaraka hizo watafikishwa katika vyombo vya dola kutokana na kuibuka kwa migogoro katika viwanja hivyo.
Waziri, Lukuvi amesema kuwa watu wenye uraia wa nje na si watanzania hawana uwezo kupata ardhi nchini na wanachotakiwa kufanya ni kupitia Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) ndio wanaweza kutoa ardhi.
Amesema kuna baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakiwaweka watanzania katika hisa na baada ya kufanikisha jambo lao la kupata ardhi wanahisa watanzania wanajitoa. Aidha amesema kuwa kiwanja kilichokuwa kinamilikiwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye kilichokuwepo Mabwepande kimefutwa umiliki kutokana na kushindwa kuendelezwa kwa muda na baadae kuvamiwa na wananchi.
Amesema serikali haitaangalia mtu usoni kwa watu kumiliki ardhi bila kuendeleza kwa muda mrefu huku kukiwa na viwanja vingine kukosa mapato yake.
No comments:
Post a Comment