WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto imetoa rai kwa viongozi wa mikoa na wilaya, wataalamu na wanajamii kutoficha taarifa ya ugonjwa wa kipindupindu kwani kufanya hivyo kunakwamisha juhudi za kuudhibiti ugonjwa huo nchini.
Aidha wizara hiyo imesema kwamba yenyewe ndiyo yenye jukumu la kutoa taarifa za ugonjwa huo,hivyo mtu mwingine kwa akitoa taarifa ni zake binafsi.
Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt.Hamisi Kigwangalla wakati akitoa taarifa ya wiki kuhusu ugonjwa kipindupindu nchini kwa waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo.
“Moja ya changamoto kubwa inayoendelea kujitokeza ni pale ambapo baadhi ya wataalamu wa ngazi mbalimbali pamoja na wanajamii wanapoficha wagonjwa na hivyo kutoa taarifa ya wagonjwa wachache kuliko uhalisia.
“ Madhara yanayoambatana na hii ni kutokuwepo kwa taarifa za kutosha zitakazoongeza juhudi za kuzuia ugonjwa kutoka katika maeneo ambayo wagonjwa hawakutolewa taarifa na hivyo kuongeza hatari ya ugonjwa kuendelea kusambaa kimnyakimnya na baadae kusababisha wagonjwa wengi kujitokeza katika maeneo hayo kwa maramoja,” alisema Dkt.Kigwangalla.
Aidha Dkt.Kigwangalla alitoa rai kwa viongozi wa hususan ngazi za mikoa na wilaya kutokutoa kauli za kutaka kuwaadhibu watendaji na viongozi wa ngazi za chini kwa kigezo cha wagonjwa kuwepo katika maeneo yao kwani kwa kufanya hivyo wataongeza kasi ya kuficha wagonjwa na kumwamisha juhudi za kupambana na ugonjwa huo.
“Sisi tutaendelea kutoa taarifa za ugonjwa huu, hata kama hawataki kukubali kama kuna kipindupindu, tunafanya hivyo kwa sababu tuna takwimu sahihi,kama hawataki kutumbuliwa majipu sisi tutayatumbua,” alisema.
Naibu Waziri huyo alifafanua hayo kufuatia baadhi ya viongozi kudai Jiji la Dar es Salaam halina mgonjwa wa kipindupindu baada ya vyombo vya habari kuripoti jiji hilo lina ugonjwa huo na wagonjwa waliokuwepo ni sita kwa mujibu wa taarifa za wizara hiyo za wiki iliyopita.
Katika taarifa hiyo ya wiki kuanzia Februari 15 hadi 21, mwaka huu, Dkt. KIgwangalla alisema jumla wagonjwa walioripotiwa kuugua ugonjwa huo ni 499, ambapo kati ya hao wagonjwa sita (6) walipoteza maisha.
Alisema tangu ugonjwa huo ulipoanza Agosti mwaka huu hadi sasa jumla 16,352 wameugua ugonjwa huo, kati ya hao 249 wamepoteza maisha.
Aliongeza kwamba kwa kipindi cha wiki hiyo, jumla ya mikoa 11 imeripotiwa kuwa na ugonjwa huo, ambapo mkoa wa Iringa ndio unaongoza kuwa idadi kubwa ya wagonjwa 143, Mwanza 94, Mara 87, Dodoma 66, Morogoro 42,Mbeya 30,Arusha 17,Dar es Salaam 14,Simiyu3,Kilimanjaro 2 na Manyara 1.
No comments:
Post a Comment